Kwa hayo Yeye anaizalisha kwa ajili yenu mimea, na mizaituni, na mitende, na mizabibu, na kila namna ya matunda. Hakika katika haya zipo ishara kwa watu wanao fikiri.
Yeye ndiye aliye ifanya bahari ikutumikieni, ili kutokana na humo mpate kula nyama laini, na mtoe humo mapambo mnayo yavaa. Na unaona marikebu zikikata maji humo, ili mtafute fadhila yake, na mpate kushukuru.
Ili wabebe mizigo yao kwa ukamilifu Siku ya Kiyama, na sehemu ya mizigo ya wale wanao wapoteza bila ya kujua. Angalia, ni maovu mno hayo wanayo yabeba!
Walipanga vitimbi walio kuwa kabla yao, Mwenyezi Mungu akayasukua majengo yao kwenye misingi, dari zikawaporomokea juu yao, na adhabu ikawajia kutoka wasipo kujua.
Kisha Siku ya Kiyama atawahizi na atasema: Wako wapi hao washirika wangu ambao kwao mkiwakutisha (Manabii) mashaka? Watasema walio pewa ilimu: Hakika leo ndiyo hizaya na adhabu itawashukia makafiri,
Ambao Malaika waliwafisha nao wamejidhulumu nafsi zao! Basi watasalimu amri, waseme: Hatukuwa tukifanya uovu wowote. (Wataambiwa): Kwani! Hakika Mwenyezi Mungu anajua sana mliyo kuwa mkiyatenda.
Na wataambiwa walio mcha Mungu: Mola wenu Mlezi kateremsha nini? Watasema: Kheri. Walio fanya wema katika dunia hii watapata wema. Na nyumba ya Akhera ni bora zaidi, na njema mno nyumba ya wachamngu.
Wanangojea jengine hawa ila Malaika wawafikie, au iwafikie amri ya Mola wako Mlezi? Kama hivyo walitenda walio kuwa kabla yao. Na Mwenyezi Mungu hakuwadhulumu, lakini walijidhulumu wenyewe.
Na washirikina wanasema: Mwenyezi Mungu angeli taka tusingeli abudu chochote badala yake, sisi wala baba zetu, wala tusingeli harimisha chochote bila ya Yeye. Kama hivyo walifanya walio kuwa kabla yao. Basi lipo lolote juu ya Mitume isipo kuwa kubalighisha kwa uwazi?
Na kwa hakika kwa kila umma tuliutumia Mtume kwamba: Muabuduni Mwenyezi Mungu, na muepukeni Shetani. Basi kati yao wapo alio waongoa Mwenyezi Mungu. Na kati yao wapo ambao ulio wathibitikia upotovu. Basi tembeeni katika ardhi, muangalie ulikuwaje mwisho wa wanao kanusha.
Na wanaapa kwa Mwenyezi Mungu ukomo wa viapo vyao kwamba Mwenyezi Mungu hatomfufua aliye kufa. Kwani! Ni ahadi iliyo juu yake kikweli; lakini watu wengi hawajui.
Na wale walio hama kwa ajili ya Mwenyezi Mungu baada ya kudhulumiwa, bila ya shaka tutawaweka duniani kwa wema; na ujira wa Akhera ni mkubwa zaidi; laiti kuwa wanajua!
Na lau kuwa Mwenyezi Mungu angeli wachukulia watu kwa mujibu wa dhulma zao, basi asingeli mwacha hapa hata mnyama mmoja. Lakini anawaakhirisha mpaka muda ulio wekwa. Na unapo fika muda wao hawatakawilia hata saa moja wala hawatatangulia.
Na wanampa Mwenyezi Mungu wanavyo vichukia wao, na ndimi zao zinasema uwongo kwamba wao watapata mema. Hapana shaka hakika wamewekewa Moto, nao wataachwa humo.
Wallahi! Sisi tulituma Mitume kwa umati zilizo kuwa kabla yako, lakini Shetani aliwapambia vitendo vyao. Kwa hivyo leo yeye ndiye rafiki yao; nao watapata adhabu chungu.
Na Mwenyezi Mungu ameteremsha maji kutoka mbinguni na kwa hayo akaihuisha ardhi baada ya kufa kwake. Kwa hakika katika hayo imo Ishara kwa watu wanao sikia.
Na hakika katika nyama hoa nyinyi mna mazingatio. Tunakunywesheni katika vile viliomo matumboni mwao, vikatoka baina ya mavi na damu, maziwa safi mazuri kwa wanywao.
Kisha kula katika kila matunda, na upite katika njia za Mola wako Mlezi zilizo fanywa nyepesi kuzipita. Na kutoka matumbo yao kinatoka kinywaji chenye rangi mbali mbali; ndani yake kina matibabu kwa wanaadamu. Hakika katika haya ipo Ishara kwa watu wanao fikiri.
Na Mwenyezi Mungu amekuumbeni; kisha anakufisheni. Na miongoni mwenu wapo wanao rudishwa kwenye umri mbaya kabisa, hata akawa asijue kitu baada ya ujuzi alio kuwa nao. Hakika Mwenyezi Mungu ndiye Mjuzi na Mweza.
Na Mwenyezi Mungu amewafadhilisha baadhi yenu kuliko wengine katika riziki. Na wale walio fadhilishwa hawarudishi riziki zao kwa wale ilio wamiliki mikono yao ya kulia ili wawe sawa katika riziki hiyo. Basi je, wanazikataa neema za Mwenyezi Mungu?
Na Mwenyezi Mungu amekuumbieni wake katika jinsi yenu, na akakujaalieni kutoka kwa wake zenu wana na wajukuu, na akakuruzukuni vitu vizuri vizuri. Basi je, wanaamini upotovu na wanazikataa neema za Mwenyezi Mungu?
Mwenyezi Mungu anapiga mfano wa mtumwa aliye milikiwa, asiye weza kitu, na mwingine tuliye mruzuku riziki njema inayo toka kwetu, naye akawa anatoa katika riziki hiyo kwa siri na dhaahiri. Je, hao watakuwa sawa? Alhamdu Lillahi! Kuhimidiwa kote ni kwa Mwenyezi Mungu. Lakini wengi wao hawajui.
Na Mwenyezi Mungu anapiga mfano wa watu wawili. Mmoja wao ni bubu, hawezi chochote, naye ni mzigo kwa bwana wake. Popote anapo muelekeza haleti kheri. Je! Huyo anaweza kuwa sawa na yule anaye amrisha uadilifu, naye yuko juu ya Njia Iliyo Nyooka?
Na siri zote za katika mbingu na ardhi ziko kwa Mwenyezi Mungu. Wala halikuwa jambo la Saa (ya Kiyama) ila kama kupepesa kwa jicho, au akali ya hivyo. Hakika Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu.
Je! Hawawaoni ndege walivyo wat'iifu katika anga la mbingu? Hapana mwenye kuwashika isipo kuwa Mwenyezi Mungu. Hakika katika haya zipo ishara kwa watu wanao amini.
Na Mwenyezi Mungu amekujaalieni majumba yenu yawe ni maskani yenu, na amekujaalieni kutokana na ngozi za wanyama nyumba mnazo ziona nyepesi wakati wa safari zenu na wakati wa kutua kwenu. Na kutokana na sufi zao na manyoya yao na nywele zao mnafanya matandiko na mapambo ya kutumia kwa muda.
Na Mwenyezi Mungu amekufanyieni vivuli katika vitu alivyo viumba, na amekufanyieni maskani milimani, na amekufanyieni nguo za kukingeni na joto, na nguo za kukingeni katika vita vyenu. Ndio hivyo anakutimizieni neema zake ili mpate kut'ii.
Na (waonye) siku tutakapo wainua mashahidi katika kila umma wakiwashuhudia kwa yanayo tokana na wao, na tutakuleta wewe uwe shahidi juu ya hao. Na tumekuteremshia Kitabu hiki kinacho bainisha kila kitu, na ni uwongofu, na rehema, na bishara kwa Waislamu.
Hakika Mwenyezi Mungu anaamrisha kufanya uadilifu, na hisani, na kuwapa jamaa; na anakataza uchafu, na uovu, na dhulma. Anakuwaidhini ili mpate kukumbuka.
Na timizeni ahadi ya Mwenyezi Mungu mnapo ahidi, wala msivunje viapo baada ya kuvithibitisha, ilihali mmekwisha mfanya Mwenyezi Mungu ndiye mdhamini wenu. Hakika Mwenyezi Mungu anayajua myatendayo.
Wala msiwe kama mwanamke anaye uzongoa uzi wake baada ya kwisha usokota ukawa mgumu. Mnavifanya viapo vyenu kuwa ni njia ya kudanganyana baina yenu kwa kuwa ati taifa moja lina nguvu zaidi kuliko jengine? Hakika Mwenyezi Mungu anakujaribuni kwa njia hiyo. Na bila ya shaka atakubainishieni Siku ya Kiyama mliyo kuwa mkikhitalifiana.
Na Mwenyezi Mungu angeli taka, kwa yakini angeli kufanyeni umma mmoja. Lakini anamwachia kupotea anaye mtaka, na anamwongoa amtakaye. Na hakika mtaulizwa kwa yale mliyo kuwa mkiyafanya.
Wala msifanye viapo vyenu ni njia ya kudanganyana baina yenu. Usije mguu ukateleza badala ya kuthibiti, na mkaonja maovu kwa sababu ya kule kuzuilia Njia ya Mwenyezi Mungu, na mkapata adhabu kubwa.
Mlivyo navyo vitakwisha na vilivyoko kwa Mwenyezi Mungu ndivyo vitakavyo bakia. Na kwa yakini Sisi tutawapa walio subiri ujira wao kwa bora ya waliyo kuwa wakiyatenda.
Na tunapo badilisha Ishara pahala pa Ishara nyengine, na Mwenyezi Mungu anajua anayo teremsha, wao husema: Wewe ni mzushi. Bali wengi wao hawajui kitu.
Sema: Ameiteremsha hii Roho takatifu kutokana na Mola wako Mlezi kwa haki, ili awathibitishe wale walio amini, na kuwa ni uwongofu, na ni bishara kwa Waislamu.
Anaye mkataa Mwenyezi Mungu baada ya kuamini kwake - isipo kuwa aliye lazimishwa na hali ya kuwa moyo wake umetua juu ya Imani, lakini aliye kifungulia kifua chake kukataa - basi hao ghadhabu ya Mwenyezi Mungu ipo juu yao, na wao watapata adhabu kubwa.
Kisha hakika Mola wako Mlezi, kwa wale walio hama makwao baada ya kuteswa, kisha wakapigania Dini na wakasubiri, bila ya shaka Mola wako Mlezi baada ya hayo ni Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu.
Na Mwenyezi Mungu amepiga mfano wa mji ulio kuwa na amani na utulivu, riziki yake ikiufikia kwa nafasi kutoka kila mahali. Lakini ukazikufuru neema za Mwenyezi Mungu; kwa hivyo Mwenyezi Mungu akauvika vazi la njaa na khofu kwa sababu ya yale waliyo kuwa wakiyafanya.
Amekuharimishieni nyamafu tu, na damu, na nyama ya nguruwe, na mnyama aliye chinjwa kwa ajili isiyo kuwa ya Mwenyezi Mungu. Lakini anaye lazimishwa bila ya kuasi, wala kuruka mipaka, basi hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe na Mwenye kurehemu.
Kisha hakika Mola wako Mlezi kwa walio tenda uovu kwa ujinga, kisha wakatubia baada ya hayo na wakatenda mema; bila ya shaka Mola wako Mlezi baada ya hayo ni Mwenye kusamehe na Mwenye kurehemu.
Hakika siku ya Sabato (Jumaamosi) waliwekewa wale walio khitalifiana kwa ajili yake. Na hakika Mola wako Mlezi bila ya shaka atahukumu baina yao Siku ya Kiyama katika yale waliyo kuwa wakikhitalifiana.
Waite waelekee kwenye Njia ya Mola wako Mlezi kwa hikima na mawaidha mema, na ujadiliane nao kwa namna iliyo bora. Hakika Mola wako Mlezi ndiye anaye mjua zaidi aliye ipotea Njia yake, na Yeye ndiye anaye wajua zaidi walio ongoka.