Enyi mlio amini! Msinyanyue sauti zenu kuliko sauti ya Nabii, wala msiseme naye kwa kelele kama mnavyo semezana nyinyi kwa nyinyi, visije vitendo vyenu vikaharibika, na hali hamtambui.
Kwa hakika wanao teremsha sauti zao mbele ya Mtume wa Mwenyezi Mungu, hao ndio Mwenyezi Mungu amezisafisha nyoyo zao kwa uchamngu. Hao watakuwa na maghfira na ujira mkubwa.
Na jueni kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu yuko nanyi. Lau angeli kut'iini katika mambo mengi, bila ya shaka mngeli taabika. Lakini Mwenyezi Mungu amekupendezeeni Imani, na akaipamba katika nyoyo zenu, na amekufanyeni muuchukie ukafiri, na upotovu, na uasi. Hao ndio walio ongoka,
Na ikiwa makundi mawili katika Waumini yanapigana, basi yapatanisheni. Na likiwa moja la hao linamdhulumu mwenzie, basi lipigeni linalo dhulumu mpaka lirejee kwenye amri ya Mwenyezi Mungu. Na likirudi basi yapatanisheni kwa uadilifu. Na hukumuni kwa haki. Hakika Mwenyezi Mungu anawapenda wanao hukumu kwa haki.
Enyi mlio amini! Wanaume wasiwadharau wanaume wenzao, wala wanawake wasiwadharau wanawake wenzao. Huenda hao wakawa bora kuliko wao. Wala msivunjiane hishima, wala msiitane kwa majina ya kejeli. Ni uovu kutumia jina baya baada ya kwisha amini. Na wasio tubu, hao ndio wenye kudhulumu.
Enyi mlio amini! Jiepusheni na dhana nyingi, kwani baadhi ya dhana ni dhambi. Wala msipelelezane, wala msisengenyane nyinyi kwa nyinyi. Je! Yupo katika nyinyi anaye penda kuila nyama ya nduguye aliye kufa? Mnalichukia hilo! Na mcheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kupokea toba, Mwenye kurehemu.
Enyi watu! Hakika Sisi tumekuumbeni kutokana na mwanamume na mwanamke. Na tumekujaalieni kuwa ni mataifa na makabila ili mjuane. Hakika aliye mtukufu zaidi kati yenu kwa Mwenyezi Mungu ni huyo aliye mchamngu zaidi katika nyinyi. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua, Mwenye khabari.
Mabedui wamesema: Tumeamini. Sema: Hamjaamini, lakini semeni: Tumesilimu. Kwani Imani haijaingia katika nyoyo zenu. Na mkimt'ii Mwenyezi Mungu na Mtume wake, hatakupunguzieni chochote katika vitendo vyenu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.
Hakika Waumini ni wale walio muamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake tena wasitie shaka kabisa, na wakapigana Jihadi katika Njia ya Mwenyezi Mungu kwa mali yao na nafsi zao. Hao ndio wakweli.
Wanakusimbulia kuwa wamesilimu! Sema: Msinisimbulie kwa kusilimu kwenu. Bali Mwenyezi Mungu ndiye aliye kufanyieni hisani kwa kukuongoeni kwenye Imani, ikiwa nyinyi ni wakweli.