Hakika Dini Safi ni ya Mwenyezi Mungu tu. Na wale wanao wafanya wenginewe kuwa ni walinzi wakisema: Sisi hatuwaabudu ila wapate kutujongeza tu kumkaribia Mwenyezi Mungu - Hakika Mwenyezi Mungu atahukumu baina yao katika wanayo khitalifiana. Hakika Mwenyezi Mungu hamwongoi aliye mwongo kafiri.
Lau kuwa Mwenyezi Mungu angeli taka kuwa na mwana, basi bila ya shaka angeli teua amtakaye katika alio waumba. Subhanahu, Ametakasika na hayo! Yeye ni Mwenyezi Mungu Mmoja, Mtenda atakalo.
Ameumba mbingu na ardhi kwa Haki. Hufunika usiku juu ya mchana, na hufunika mchana juu ya usiku. Na amefanya jua na mwezi vitumike. Kila kimojapo kinakwenda kwa kipindi kilicho wekewa. Jueni mtanabahi! Yeye ndiye Mwenye nguvu, Mwenye kusamehe!
Amekuumbeni kutokana na nafsi moja. Kisha akamfanya mwenziwe katika nafsi ile ile. Na akakuleteeni wanyama wa mifugo jozi nane. Anakuumbeni katika matumbo ya mama zenu, umbo baada ya umbo, katika viza vitatu. Huyu ndiye Mwenyezi Mungu Mola wenu Mlezi. Ufalme ni wake. Hapana mungu isipo kuwa Yeye. Basi nyinyi mnageuzwa wapi?
Mkikufuru basi Mwenyezi Mungu si mwenye haja nanyi, lakini hafurahii kufuru kwa waja wake. Na mkishukuru Yeye hufurahika nanyi. Wala mbebaji habebi mzigo wa mwingine. Kisha marejeo yenu ni kwa Mola wenu Mlezi. Hapo atakwambieni mliyo kuwa mkiyafanya. Hakika Yeye ni Mwenye kuyajua vyema yaliyomo vifuani.
Na taabu inapo mfikia mtu humwomba Mola wake Mlezi naye ameelekea kwake. Kisha akimpa neema kutoka kwake, husahau yale aliyo kuwa akimwitia zamani, na akamfanyia Mwenyezi Mungu washirika ili apoteze watu njia yake. Sema: Starehe na ukafiri wako kwa muda mchache. Kwani hakika wewe utakuwa miongoni mwa watu wa Motoni.
Je! Afanyae ibada nyakati za usiku kwa kusujudu na kusimama akitahadhari na Akhera, na akitaraji rehema za Mola wake Mlezi... Sema: Ati watakuwa sawa wale wanao jua na wale wasio jua? Hakika wanao kumbuka ni watu wenye akili.
Sema: Enyi waja wangu mlio amini! Mcheni Mola wenu Mlezi. Wale wafanyao wema katika dunia hii watapata wema. Na ardhi ya Mwenyezi Mungu ni kunjufu. Hakika wenye subira watapewa ujira wao bila ya hisabu.
Basi nyinyi abuduni mpendacho badala yake Yeye. Sema: Hakika walio khasirika ni wale walio jikhasiri nafsi zao na ahali zao Siku ya Kiyama. Tambueni kuwa hiyo ndiyo khasara iliyo dhaahiri.
Lakini walio mcha Mola wao Mlezi watapata ghorofa zilizo jengwa juu ya ghorofa; chini yake hupita mito. Ndiyo ahadi ya Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu havunji ahadi yake.
Je! Huoni kwamba Mwenyezi Mungu ameteremsha maji kutoka mbinguni. Kisha akayapitisha kwenye chemchem katika ardhi, kisha kwa maji hayo akatoa mimea yenye rangi mbali mbali? Kisha hunyauka ukaiona imekuwa kimanjano, na kisha huifanya mapepe. Bila ya shaka katika hayo upo ukumbusho kwa wenye akili.
Je! Yule ambaye Mwenyezi Mungu amemfungulia kifua chake kwa Uislamu, na akawa yuko kwenye nuru itokayo kwa Mola wake Mlezi (ni sawa na mwenye moyo mgumu?) Basi ole wao wenye nyoyo ngumu zisio mkumbuka Mwenyezi Mungu! Hao wamo katika upotofu wa dhaahiri.
Mwenyezi Mungu ameteremsha hadithi nzuri kabisa, Kitabu chenye kufanana na kukaririwa; husisimua kwacho ngozi za wenye kumkhofu Mola wao Mlezi. Kisha ngozi zao na nyoyo zao hulainika kwa kumkumbuka Mwenyezi Mungu. Huo ndio uwongofu wa Mwenyezi Mungu, na kwa huo humwongoa amtakaye. Na ambaye ameachwa na Mwenyezi Mungu kupotea, basi hapana wa kumwongoa.
Je! Atakaye kuwa anapambana kwa uso wake na adhabu mbaya kabisa Siku ya Kiyama (ni sawa na watenda wema?) Na wataambiwa wenye kudhulumu: Onjeni hayo mliyo kuwa mkiyachuma!
Mwenyezi Mungu amepiga mfano wa mtu mwenye mabwana washirika wanao gombana, na wa mtu mwengine aliye khusika na bwana mmoja tu. Je! Wako sawa katika hali zao? Alhamdulillahi, Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu! Lakini wengi wao hawajui.
BASI NI NANI dhaalimu mkubwa kuliko yule aliye msingizia uwongo Mwenyezi Mungu na kuikanusha kweli imfikiapo? Je! Siyo katika Jahannamu makaazi ya hao makafiri?
Je! Mwenyezi Mungu si wa kumtosheleza mja wake? Na ati wanakutishia kwa hao wenginewe wasio kuwa Yeye! Na aliye hukumiwa na Mwenyezi Mungu kupotea hana wa kumwongoa.
Na ukiwauliza: Ni nani aliye ziumba mbingu na ardhi. Bila ya shaka watasema: Mwenyezi Mungu. Sema: Je! Mnawaonaje wale mnao waomba badala ya Mwenyezi Mungu, ikiwa Mwenyezi Mungu akitaka kunidhuru, wao wanaweza kuniondolea dhara yake? Au akitaka kunirehemu, je, wao wanaweza kuzuia rehema yake? Sema: Mwenyezi Mungu ananitosheleza. Kwake Yeye wategemee wanao tegemea.
Hakika Sisi tumekuteremshia Kitabu kwa ajili ya watu wote kwa Haki. Basi mwenye kuongoka ni kwa nafsi yake, na mwenye kupotoka bila ya shaka amepotoka kwa khasara yake. Na wewe si mlinzi juu yao.
MWENYEZI MUNGU huzipokea roho zinapo kufa. Na zile zisio kufa wakati wa kulala kwake, huzishika zilizo hukumiwa kufa, na huzirudisha nyengine mpaka ufike wakati uliowekwa. Hakika katika hayo bila ya shaka zipo Ishara kwa watu wanao fikiri.
Sema: Ewe Mwenyezi Mungu! Muumba mbingu na ardhi! Mjuzi wa yasiyo onekana na yanayo onekana! Wewe utahukumu baina ya waja wako katika waliyo kuwa wakikhitalifiana.
Na lau kuwa walio dhulumu wangeli kuwa na vyote viliomo duniani na pamoja navyo vingine kama hivyo, bila ya shaka wangeli vitoa kujikomboa katika adhabu mbaya hiyo Siku ya Kiyama. Na yatawadhihirikia kwa Mwenyezi Mungu wasiyo kuwa wakiyatarajia.
Na dhara inapo mgusa mtu hutuomba. Kisha tunapo mpa neema zitokazo kwetu, husema: Nimepewa haya kwa sababu ya ilimu yangu. Sio! Huo ni mtihani! Lakini wengi wao hawajui!
Sema: Enyi waja wangu walio jidhulumu nafsi zao! Msikate tamaa na rehema ya Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu husamehe dhambi zote. Hakika Yeye ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.
Na kwa yakini yamefunuliwa kwako na kwa walio kuwa kabla yako: Bila ya shaka ukimshirikisha Mwenyezi Mungu a'mali zako zitaanguka, na lazima utakuwa miongoni mwa wenye kukhasiri.
Na wala hawakumhishimu Mwenyezi Mungu kama anavyo stahiki kadiri yake. Na Siku ya Kiyama ardhi yote itakuwa mkononi mwake, na mbingu zitakunjwa katika mkono wake wa kuume. Subhanahu wa Taa'la Ametakasika na Ametukuka na hayo wanayo mshirikisha nayo.
Na litapulizwa barugumu, wazimie waliomo mbinguni na waliomo katika ardhi, isipo kuwa aliye mtaka Mwenyezi Mungu. Kisha litapulizwa mara nyengine. Hapo watainuka wawe wanangojea.
Na ardhi itang'ara kwa Nuru ya Mola wake Mlezi, na Kitabu kitawekwa, na wataletwa Manabii na mashahidi, na patahukumiwa baina yao kwa haki, wala hawatadhulumiwa.
Na walio kufuru wataongozwa kuendea Jahannamu kwa makundi. Mpaka watakapo ifikia itafunguliwa milango yake, na walinzi wake watawaambia: Kwani hawakukujilieni Mitume miongoni mwenu wakikusomeeni Aya za Mola wenu Mlezi na kukuonyeni mkutano wa siku yenu hii? Watasema: Kwani! Lakini limekwisha thibiti neno la adhabu juu ya makafiri.
Na walio mcha Mola wao Mlezi wataongozwa kuendea Peponi kwa makundi, mpaka watakapo fikilia, nayo milango yake imekwisha funguliwa. Walinzi wake watawaambia: Salaam Alaikum, Amani iwe juu yenu! Mmet'ahirika. Basi ingieni humu mkae milele.
Nao watasema: Alhamdulillah, Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu aliye tutimizia ahadi yake, na akaturithisha ardhi, tunakaa katika Bustani popote tupendapo. Basi ni malipo mazuri yaliyoje ya watendao!
Na utawaona Malaika wakizunguka pembeni mwa Kiti cha enzi cha Mwenyezi Mungu, wakimtakasa na kumsifu Mola wao Mlezi. Na patahukumiwa baina yao kwa haki na patasemwa: Sifa zote njema ni za Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa viumbe vyote!