Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, ambaye ni vyake vyote viliomo mbnguni na katika ardhi. Na sifa ni zake Yeye katika Akhera. Naye ni Mwenye hikima, Mwenye khabari.
Anajua yanayo ingia katika ardhi na yanayo toka humo, na yanayo teremka kutoka mbinguni, na yanayo panda huko. Na Yeye ni Mwenye kurehemu, Mwenye kusamehe.
Na walisema walio kufuru: Haitatufikia Saa (ya Kiyama). Sema: Kwani? Hapana shaka itakufikieni, naapa kwa haki ya Mola wangu Mlezi, Mwenye kujua ya ghaibu! Hapana kinacho fichikana kwake hata chenye uzito wa chembe tu, si katika mbingu wala katika ardhi, wala kilicho kidogo kuliko hivyo, wala kikubwa zaidi; ila vyote hivyo vimo katika Kitabu chake chenye kubainisha.
Kwani hawaoni yaliyo mbele yao na yaliyo nyuma yao ya mbingu na ardhi? Tungeli penda tungeli wadidimiza ndani ya ardhi, au tungeli wateremshia juu yao vipande vya mbingu. Hakika katika haya zipo Ishara kwa kila mja aliye tubia.
Na Suleiman tuliufanya upepo umtumikie. Safari yake ya asubuhi ni mwendo wa mwezi mmoja, na safari yake ya jioni ni mwendo wa mwezi mmoja. Na tukamyayushia chemchem ya shaba. Na katika majini walikuwako walio kuwa wakifanya kazi mbele yake kwa idhini ya Mola wake Mlezi. Na kila anaye jitenga na amri yetu katika wao, tunamwonjesha adhabu ya Moto unao waka.
Walikuwa wakimfanyia alipendalo, kama mihrabu, na masanamu, na madeste makubwa kama mahodhi, na masufuria makubwa yasiyo ondolewa mahala pake. Enyi watu wa Daudi! Fanyeni kazi kwa kushukuru. Ni wachache katika waja wangu wanao shukuru.
Na tulipo mhukumia kufa, hapana aliye wajuulisha kufa kwake ila mnyama wa ardhi aliye kula fimbo yake. Na alipo anguka majini walitambua lau kuwa wangeli jua ya ghaibu wasingeli kaa katika adhabu hiyo ya kufedhehesha.
Hakika ilikuwapo Ishara kwa (watu wa nchi ya) Sabaa katika maskani yao - bustani mbili, kulia na kushoto. Kuleni katika riziki ya Mwenyezi Mungu, na mumshukuru. Mji mzuri na Mola Mlezi aliye Msamehevu.
Lakini wakaacha. Tukawapelekea mafuriko makubwa, na tukawabadilishia badala ya bustani zao hizo kwa bustani nyengine zenye matunda makali machungu, na mivinje, na kidogo katika miti ya kunazi.
Na baina yao na miji mingine tuliyo ibariki tuliweka miji iliyo dhaahiri, na tukaweka humo vituo vya safari. Tukawaambia: Nendeni humo usiku na mchana kwa amani.
Lakini wakasema: Mola wetu Mlezi! Weka mwendo mrefu baina ya safari zetu. Na wakazidhulumu nafsi zao. Basi tukawafanya ni masimulizi tu, na tukawatawanya tawanya. Hakika katika hayo bila ya shaka zimo Ishara kwa kila mwenye kusubiri sana na akashukuru.
Na yeye hakuwa na mamlaka yoyote juu yao, ila kwa sababu ya kuwajaribu tujue nani mwenye kuamini Akhera, na nani anaye tilia shaka. Na Mola wako Mlezi ni Mwenye kuhifadhi kila kitu.
Sema: Waite mnao wadaia kuwa ni badala ya Mwenyezi Mungu. Hawamiliki hata uzito wa chembe hichi katika mbingu wala ardhi. Wala hawana ushirika wowote humo. Wala Yeye hana msaidizi miongoni mwao.
Wala uombezi mbele yake hautafaa kitu, isipo kuwa kwa aliye mpa idhini. Hata itapo ondolewa khofu kwenye nyoyo zao watasema: Mola wenu Mlezi kasema nini? Watasema: Yaliyo kweli! Na Yeye ndiye Aliye juu, Mkubwa.
Sema: Ni nani anaye kuruzukuni kutoka mbinguni na kwenye ardhi? Sema: Mwenyezi Mungu! Na hakika sisi au nyinyi bila ya shaka tuko kwenye uwongofu au upotofu ulio wazi.
Na walisema walio kufuru: Hatutaiamini Qur'ani hii, wala yaliyo kuwa kabla yake. Na ungeli waona madhaalimu watapo simamishwa mbele ya Mola wao Mlezi, wakirudishiana maneno wao kwa wao! Wanyonge wakiwaambia walio takabari: Lau kuwa si nyinyi, bila ya shaka tungeli kuwa Waumini sisi.
Na wanyonge wakawaambia walio takabari: Bali ni vitimbi vyenu vya usiku na mchana, mlipo kuwa mkituamrisha tumkufuru Mwenyezi Mungu, na tumfanyie washirika. Nao wataficha majuto watakapo iona adhabu. Na tutaweka makongwa shingoni mwao walio kufuru. Kwani wanalipwa ila kwa waliyo kuwa wakiyatenda?
Na si mali yenu wala watoto wenu watakao kukaribisheni kwetu muwe karibu, isipo kuwa aliye amini na akatenda mema. Hao basi watapata malipo mardufu kwa walio yafanya. Nao watakuwa salama katika maghorofa.
Sema: Kwa hakika Mola wangu Mlezi humkunjulia riziki na humdhikisha amtakaye katika waja wake. Na chochote mtakacho kitoa Yeye atakilipa. Naye ni Mbora wa wanao ruzuku.
Na wanapo somewa Aya zetu zilizo wazi wanasema: Huyu si chochote ila ni mtu anaye taka kukuzuieni na waliyo kuwa wakiabudu baba zenu. Na wakasema: Haya si chochote ila ni uwongo ulio zuliwa. Na walio kufuru waliiambia Haki ilipo wajia: Haya si chochote ila ni uchawi ulio dhaahiri.
Na walikadhibisha walio kuwa kabla yao. Na hawakufikilia hata sehemu moja katika kumi ya tulivyo wapa hao. Nao waliwakadhibisha Mitume wangu. Basi kuangamiza kwangu kulikuwa namna gani!
Sema: Mimi nakunasihini kwa jambo moja tu - ya kwamba msimame kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, wawili-wawili na mmoja-mmoja; kisha mfikiri. Mwenzenu huyu hana wazimu. Yeye si chochote ila ni Mwonyaji kwenu kabla ya kufika adhabu kali.
Sema: Ikiwa mimi nimepotea, basi nimepotea kwa kudhuru nafsi yangu mwenyewe. Na ikiwa nimeongoka, basi ni kwa sababu ya kunifunulia Mola wangu Mlezi. Hakika Yeye ni Mwenye kusikia, Aliye karibu.