Na tumemuusia mwanaadamu kuwafanyia wema wazazi wake. Na ikiwa watakushikilia unishirikishe Mimi na usiyo kuwa na ujuzi nayo, basi usiwat'ii. Kwangu Mimi ndio marejeo yenu, na nitakwambieni mliyo kuwa mkiyatenda.
Na katika watu wapo wanao sema: Tumemuamini Mwenyezi Mungu. Lakini wanapo pewa maudhi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, wanayafanya mateso ya watu kama ni adhabu ya Mwenyezi Mungu. Na inapo kuja nusura kutoka kwa Mola wako Mlezi husema: Hakika sisi tulikuwa pamoja nanyi. Kwani Mwenyezi Mungu hayajui yaliomo vifuani mwa walimwengu?
Na walio kufuru waliwaambia walio amini: Fuateni njia yetu, nasi tutayabeba makosa yenu. Wala wao hawatabeba katika makosa yao chochote kile. Hakika hao ni waongo.
Hakika nyinyi mnaabudu masanamu badala ya Mwenyezi Mungu, na mnazua uzushi. Hakika hao mnao waabudu badala ya Mwenyezi Mungu hawakumilikiini riziki yoyote. Takeni riziki kwa Mwenyezi Mungu, na mumuabudu Yeye, na mumshukuru Yeye. Kwake Yeye ndio mtarudishwa.
Sema: Tembeeni katika ardhi na tazameni jinsi alivyo anzisha uumbaji; kisha Mwenyezi Mungu ndiye anaye umba umbo la baadaye. Hakika Mwenyezi Mungu ni Muweza juu ya kila kitu.
Basi haikuwa jawabu ya watu wake ila ni kusema: Muuweni au mchomeni moto! Mwenyezi Mungu akamwokoa na moto. Hakika katika hayo zipo Ishara kwa watu wanao amini.
Na alisema: Hakika nyinyi mmeyashika masanamu badala ya Mwenyezi Mungu kwa mapenzi yaliyo baina yenu katika uhai wa duniani. Kisha Siku ya Kiyama mtakataana nyinyi kwa nyinyi, na mtalaaniana nyinyi kwa nyinyi. Na makaazi yenu ni Motoni. Wala hamtapata wa kukunusuruni.
Na tulimtunukia (Ibrahim) Is-haq na Yaa'qub. Na tukajaalia katika dhuriya zake Unabii na Kitabu, na tukampa ujira wake katika dunia; naye hakika katika Akhera bila ya shaka ni katika watu wema.
Je! Nyinyi mnawaingilia wanaume, na mnaikata njia? Na katika mikutano yenu mnafanya maovu? Basi haikuwa jawabu ya watu wake isipo kuwa kusema: Tuletee hiyo adhabu ya Mwenyezi Mungu ikiwa wewe ni katika wasemao kweli.
Na wajumbe wetu walipo mjia Ibrahim na bishara, walisema: Hakika sisi hapana shaka tutawahiliki watu wa mji huu, kwani watu wake hakika wamekuwa madhaalimu.
Akasema: Hakika humo yumo Lut'i. Wao wakasema: Sisi tunajua zaidi nani yumo humo. Hapana shaka tutamwokoa yeye na ahali zake, isipo kuwa mkewe aliye miongoni mwa watao kaa nyuma.
Na wajumbe wetu walipo mfikia Lut'i, alihuzunika kwa ajili yao, na moyo uliona dhiki kwa ajili yao. Wakasema: Usiogope, wala usihuzunike. Hakika sisi tutakuokoa wewe na ahali zako, ila mkeo aliye miongoni mwa watao kaa nyuma.
Na kwa Madyana tulimtuma ndugu yao Shuaibu, naye akasema: Enyi watu wangu! Muabuduni Mwenyezi Mungu na iogopeni Siku ya Akhera, wala msende katika ardhi mkifisidi.
Na pia kina A'di na Thamud. Nanyi yamekwisha kubainikieni kutokana na maskani zao. Na Shet'ani aliwapambia vitendo vyao, na akawazuilia Njia, na hali walikuwa wenye kuona.
Basi kila mmoja tulimtesa kwa mujibu wa makosa yake. Kati yao wapo tulio wapelekea kimbunga cha changarawe; na kati yao wapo walio nyakuliwa na ukelele; na kati yao wapo ambao tulio wadidimiza katika ardhi; na kati yao wapo tulio wazamisha. Wala Mwenyezi Mungu hakuwa mwenye kuwadhulumu, lakini walikuwa wenyewe wakijidhulumu nafsi zao.
Mfano wa walio wafanya walinzi badala ya Mwenyezi Mungu, ni mfano wa buibui alivyo jitandia nyumba. Na hakika nyumba dhaifu mno kuliko zote ni jumba la buibui, laiti kuwa wanajua.
SOMA uliyo funuliwa katika Kitabu, na ushike Sala. Hakika Sala inazuilia mambo machafu na maovu. Na kwa yakini kumdhukuru Mwenyezi Mungu ndilo jambo kubwa kabisa. Na Mwenyezi Mungu anayajua mnayo yatenda.
Wala msijadiliane na Watu wa Kitabu ila kwa njia iliyo nzuri kabisa, isipo kuwa wale walio dhulumu miongoni mwao. Na semeni: Tumeyaamini yaliyo teremshwa kwetu na yaliyo teremshwa kwenu. Na Mungu wetu na Mungu wenu ni Mmoja. Na sisi ni wenye kusilimu kwake.
Na namna hivi tumekuteremshia Kitabu (cha Qur'ani). Basi wale tulio wapa Kitabu (cha Biblia) wataiamini (Qur'ani), na miongoni mwa hawa (washirikina) wapo watakao iamini. Na hawazikatai Ishara zetu isipo kuwa makafiri.
Na walisema: Mbona hakuteremshiwa Ishara kutoka kwa Mola wake Mlezi? Sema: Ishara ziko kwake Mwenyezi Mungu; ama mimi kwa hakika ni mwonyaji mwenye kubainisha tu.
Sema: Mwenyezi Mungu anatosha kuwa ni Shahidi baina yangu na nyinyi. Anayajua yaliomo katika mbingu na ardhi. Na wale wanao amini upotovu na wakamkataa Mwenyezi Mungu, hao ndio walio khasiri.
Na wanakuhimiza waletewe adhabu kwa haraka. Na lau kuwa hapana wakati maalumu ulio wekwa, basi adhabu ingeli wajia, na ingeli watokea kwa ghafla, na hali wao hawana khabari.
Na ambao wameamini na wakatenda mema, bila ya shaka tutawaweka katika maghorofa ya Peponi yenye kupitiwa chini yake mito, wakidumu humo. Ni mwema ulioje huo ujira wa watendao, Â
Na ukiwauliza; Nani aliye umba mbingu na ardhi na akafanya jua na mwezi kuti'ii amri yake? Bila ya shaka, watasema: Mwenyezi Mungu. Wapi basi wanako geuzwa?
Na ukiwauliza: Ni nani anaye teremsha maji kutoka mbinguni, na akaihuisha ardhi baada ya kufa kwake? Bila ya shaka watasema: Ni Mwenyezi Mungu. Sema: Alhamdu Lillahi, Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu. Bali wengi katika wao hawafahamu.
Je! Hawaoni ya kwamba tumeifanya nchi takatifu ina amani, na hali watu wengine wananyakuliwa kote kwa majirani zao? Je! Wanaamini upotovu, na neema za Mwenyezi Mungu wanazikataa?
Na nani dhaalimu mkubwa kuliko yule anaye mzulia uwongo Mwenyezi Mungu au anaye kanusha Haki inapo mjia? Je! Si katika Jahannamu ndio yatakuwa makaazi ya makafiri?