Hakika Firauni alitakabari katika nchi, na akawagawa wananchi makundi mbali mbali. Akalidhoofisha taifa moja miongoni mwao, akiwachinja watoto wao wanaume na akiwaacha watoto wao wanawake. Hakika yeye alikuwa katika mafisadi.
Tulimfunulia mama yake Musa kwa kumwambia: Mnyonyeshe. Na utakapo mkhofia basi mtie mtoni, na usikhofu wala usihuzunike. Hakika Sisi tutamrudisha kwako na tutamfanya miongoni mwa Mitume.
Na tukamjaalia awakatae wanyonyeshaji wote tangu mwanzo, mpaka dada yake akasema: Je! Nikuonyesheni watu wa nyumba watakao mlea kwa ajili yenu, nao pia watakuwa wema kwake?
Basi tukamrudisha kwa mama yake ili macho yake yaburudike, wala asihuzunike. Na ajue ya kwamba ahadi ya Mwenyezi Mungu ni ya kweli, lakini wengi wao hawajui.
Na akaingia mjini wakati wa kughafilika wenyeji wake, na akakuta humo watu wawili wanapigana - mmoja ni katika wenzake, na mwengine katika maadui zake. Yule mwenzake alimtaka msaada kumpiga adui yake. Musa akampiga ngumi, akamuuwa. Akasema: Hiki ni kitendo cha Shet'ani; hakika yeye ni adui, mpotezaji dhaahiri.
Akapambazukiwa mjini asubuhi naye ana khofu, akiangalia huku na huku. Mara yule yule aliye mtaka msaada jana akawa anampigia kelele amsaidie. Musa akamwambia: Hakika wewe ni mgomvi kweli kweli.
Basi alipo taka kumshika kwa nguvu yule aliye adui wao wote wawili, akasema: Ewe Musa! Unataka kuniuwa kama ulivyo muuwa mtu jana? Wewe hutaki ila kuwa jabari katika nchi, wala hutaki kuwa miongoni mwa wenye maslaha..
Na alipo yafikia maji ya Madyana alikuta umati wa watu wananywesha (wanyama wao), na akakuta karibu yao wanawake wawili wanawazuia wanyama wao. Akasema: Mna nini? Wakasema: Hatunyweshi sisi mpaka wamalize hao wachunga. Na baba yetu ni mzee sana.
Basi mmoja katika wale wanawake wawili akamjia, naye anaona haya. Akasema: Baba yangu anakwita akulipe ujira wa kutunyweshea. Basi alipo mjia na akamsimulia visa vyake, alisema: Usiogope; umekwisha okoka kwenye watu madhaalimu.
Akasema: Mimi nataka kukuoza mmojawapo katika binti zangu hawa wawili kwa kunitumikia miaka minane. Ukitimiza kumi, khiari yako; lakini mimi sitaki kukutaabisha. Inshallah utanikuta miongoni mwa watu wema.
Musa akasema: Hayo yamekwisha kuwa baina yangu na wewe. Muda mmojapo nikiumaliza sitiwi ubayani. Na Mwenyezi Mungu ni Mlinzi juu ya haya tunayo yasema.
Basi alipo timiza muda wake na akasafiri na ahali zake, aliona moto upande wa Mlima T'uri. Akawaambia ahali zake: Ngojeni! Mimi nimeona moto, labda nitakuleteeni kutoka huko khabari au kijinga cha moto ili mpate kuota moto.
Basi alipo ufikia aliitwa kutoka ng'ambo ya bonde la kuliani katika eneo lilio barikiwa kutoka kwenye mti: Ewe Musa! Hakika Mimi ni Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa walimwengu wote.
Na tupa chini fimbo yako. Basi alipo iona ikitikisika kama nyoka, akarudi nyuma wala hakutazama. (Akaambiwa): Ewe Musa! Njoo mbele wala usiogope. Hakika wewe ni miongoni mwa walio salimika.
Ingiza mkono wako kwenye mfuko wako, utatoka mweupe pasipo na ubaya. Na jiambatishe mkono wako ukihisi khofu. Basi hizi ni dalili mbili zitokazo kwa Mola wako Mlezi kumpelekea Firauni na wakuu wa umma wake. Hakika hao walikuwa watu mafaasiki.
Na ndugu yangu Harun ni fasihi zaidi ulimi wake kuliko mimi. Basi mtume ende nami kunisaidia, ili anisadikishe. Hakika mimi nina khofu watanikadhibisha.
(Mwenyezi Mungu) akasema: Tutautia nguvu mkono wako kwa nduguyo, na tutakupeni madaraka, hata wasikufikilieni. Kwa sababu ya Ishara zetu nyinyi na watakao kufuateni mtashinda.
Na Musa akasema: Mola wangu Mlezi ni Mwenye kujua kabisa nani anaye kuja na uwongofu unao toka kwake, na nani atakaye kuwa na mwisho mwema wa makaazi. Hakika wenye kudhulumu hawatafanikiwa.
Na Firauni akasema: Enyi waheshimiwa! Sijui kama mnaye mungu asiye kuwa mimi. Ewe Haman! Niwashie moto unichomee udongo, unijengee mnara nipate kumchungulia mungu wa Musa. Na hakika mimi namwona yeye ni katika waongo.
Na hakika bila ya shaka tulimpa Musa Kitabu baada ya kwisha ziangamiza kaumu za mwanzo, ili kiwafumbue macho watu, na kiwe uwongofu, na rehema, ili wapate kukumbuka.
Lakini Sisi tuliziumba kaumu, na ukawa mrefu umri juu yao. Wala hukuwa mkaazi na watu wa Madyana ukiwasomea Aya zetu. Lakini ni Sisi tulio kuwa tukiwatuma Mitume.
Wala hukuwa kando ya mlima tulipo nadi. Lakini ni rehema itokayo kwa Mola wako Mlezi ili uwaonye watu wasio pata kufikiwa na mwonyaji kabla yako, huenda wakakumbuka.
Ilipo wajia Haki kutoka kwetu walisema: Mbona hakupewa kama aliyo pewa Musa? Je! Kwani wao hawakuyakataa aliyo pewa Musa zamani? Walisema: Ni wachawi wawili wanasaidiana. Na wakasema: Hakika sisi tunawakataa wote.
Na ikiwa hawakuitikii, basi jua kuwa wanafuata pumbao lao tu. Na nani aliye potea zaidi kumshinda anaye fuata pumbao lake bila ya uwongofu utokao kwa Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu hawaongoi watu wenye kudhulumu.
Na wanapo somewa wanasema: Tunaiamini. Hakika hii ni Haki inayo toka kwa Mola wetu Mlezi. Hakika sisi kabla yake tulikuwa ni Waislamu, tulio nyenyekea.
Na wanapo sikia upuuzi hujitenga nao na husema: Sisi tuna vitendo vyetu, na nyinyi mna vitendo vyenu. Salamun Alaikum, Amani juu yenu! Sisi hatutaki kujibizana na wajinga.
Na wakasema: Tukiufuata uwongofu huu pamoja nawe tutanyakuliwa kutoka nchi yetu. Je! Kwani Sisi hatukuwaweka imara katika pahala patakatifu, penye amani, ambapo huletewa matunda ya kila aina kuwa ni riziki itokayo kwetu? Lakini wengi wao hawajui.
Na miji mingapi iliyo jifakharisha tumeiangamiza! Na hayo maskani yao hayakukaliwa tena baada yao, ila kwa uchache tu. Na Sisi ndio tumekuwa warithi wao.
Na Mola wako Mlezi haangamizi miji mpaka ampeleke Mtume katika miji yake mikuu awasomee Ishara zetu. Wala hatuiangamizi miji mpaka watu wake wawe madhaalimu.
Na chochote mlicho pewa ni matumizi ya maisha ya dunia na pambo lake. Na yaliyoko kwa Mwenyezi Mungu ndio bora na yatakayo baki zaidi. Basi je, hamfahamu?
Je! Yule tuliye muahidi ahadi nzuri, tena naye akayapata, ni kama tuliye mstarehesha kwa starehe za maisha ya duniani, na kisha Siku ya Kiyama akawa miongoni mwa wanao hudhurishwa?
Naye ni Mwenyezi Mungu ambaye hapana mungu isipo kuwa Yeye. Sifa zote njema ni zake Yeye, mwanzo na mwisho. Na hukumu ni yake Yeye. Na kwake Yeye mtarejeshwa.
Sema: Mwaonaje, Mwenyezi Mungu angeli ufanya usiku umekukalieni moja kwa moja mpaka Siku ya Kiyama, mungu gani asiye kuwa Mwenyezi Mungu atakaye kuleteeni mwangaza? Basi je, hamsikii?
Sema: Mwaonaje, Mwenyezi Mungu angeli ufanya mchana umekukalieni moja kwa moja mpaka Siku ya Kiyama, mungu gani asiye kuwa Mwenyezi Mungu ataye kuleteeni usiku mkapumzika humo? Basi je, hamwoni?
Na tutatoa shahidi katika kila umma, na tutasema: Leteni hoja zenu! Hapo watajua kwamba hakika kweli ni ya Mwenyezi Mungu, na yatawapotea yale waliyo kuwa wakiyazua.
Hakika Qaruni alikuwa katika watu wa Musa, lakini aliwafanyia dhulma. Na tulimpa khazina ambazo funguo zake zinawatopeza watu wenye nguvu kuzichukua. Walipo mwambia watu wake: Usijigambe! Hakika Mwenyezi Mungu hawapendi wanao jigamba.
Na utafute, kwa aliyo kupa Mwenyezi Mungu, makaazi ya Akhera. Wala usisahau fungu lako la dunia. Nawe fanya wema kama Mwenyezi Mungu alivyo kufanyia wema wewe. Wala usitafute kufanya ufisadi katika ardhi. Hakika Mwenyezi Mungu hawapendi mafisadi.
Akasema: Kwa hakika nimepewa haya kwa sababu ya ilimu niliyo nayo. Je! Hakujua kwamba Mwenyezi Mungu kesha waangamiza, katika vizazi vya walio kabla yake, watu walio kuwa wenye ngubvu zaidi kuliko yeye, na wenye makundi makubwa zaidi kuliko yake. Na wakosefu hawataulizwa khabari ya dhambi zao.
Basi akawatokea watu wake katika pambo lake. Wakasema wale walio kuwa wanataka maisha ya duniani: Laiti tungeli kuwa tunayo kama aliyo pewa Qaruni! Hakika yeye ni mwenye bahati kubwa.
Na wakasema wale walio pewa ilimu: Ole wenu! Malipo ya Mwenyezi Mungu ni bora kwa mwenye kuamini na akatenda mema. Wala hawatapewa hayo isipo kuwa wenye subira.
Basi tukamdidimiza yeye na nyumba yake katika ardhi; wala halikuwepo kundi lolote la kumnusuru kwa Mwenyezi Mungu, wala hakuwa miongoni mwa wanao jitetea.
Na wale walio tamani kuwa pahala pake jana, wakawa wanasema: Kumbe Mwenyezi Mungu humkunjulia riziki amtakaye katika waja wake, na humdhikisha amtakaye. Ingeli kuwa Mwenyezi Mungu hakutufanyia hisani angeli tudidimiza. Kumbe makafiri hawafanikiwi!
Hakika aliye kulazimisha kuifuata Qur'ani hapana shaka atakurudisha pahala pa marejeo. Sema: Mola wangu Mlezi ndiye anaye mjua zaidi mwenye kuja na uwongofu, na nani aliyomo katika upotofu ulio dhaahiri.
Wala usimwombe pamoja na Mwenyezi Mungu mungu mwenginewe. Hapana mungu ila Yeye. Kila kitu kitaangamia isipo kuwa Yeye. Hukumu iko kwake, na kwake mtarejezwa.