Swahili

Surah Al-Maidah ( The Table spread with Food ) - Aya count 120
Share
Enyi mlio amini! Msivunje hishima ya alama ya Dini ya Mwenyezi Mungu wala mwezi mtakatifu, wala wanyama wanao pelekwa Makka kuchinjwa, wala vigwe vyao, wala wanao elekea kwendea Nyumba Takatifu, wakitafuta fadhila na radhi za Mola wao Mlezi. Na mkisha toka Hija yenu basi windeni. Wala kuwachukia watu kwa kuwa wali- kuzuilieni kufika Msikiti mtakatifu kusikupelekeeni kuwafanyia uadui. Na saidianeni katika wema na uchamngu. Wala msisaidiane katika dhambi na uadui. Na mcheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mkali wa kuadhibu.
Mmeharimishiwa nyamafu, na damu, na nyama ya nguruwe, na mnyama aliye chinjwa si kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, na aliye kufa kwa kunyongeka koo, na aliye kufa kwa kupigwa, na aliye kufa kwa kuanguka, na aliye kufa kwa kupigwa pembe, aliye liwa na mnyama, ila mkimdiriki kumchinja. Na pia ni haramu kula nyama aliye chinjiwa masanamu. Na ni haramu kupiga ramli. Hayo yote ni upotovu. Leo walio kufuru wamekata tamaa na Dini yenu; basi msiwaogope, bali niogopeni Mimi. Leo nimekukamiliishieni Dini yenu, na nimekutimizieni neema yangu, na nimekupendeleeni UISLAMU uwe ndiyo Dini. Na mwenye kushurutishwa na njaa, bila ya kupendelea dhambi, basi hakika Mwenyezi Mungu ni Msamehevu na Mwenye kurehemu.
Enyi mlio amini! Mnapo simama kwa ajili ya Sala basi osheni nyuso zenu, na mikono yenu mpaka vifundoni, na mpake vichwa vyenu, na osheni miguu yenu mpaka vifundoni. Na mkiwa na janaba basi ogeni. Na mkiwa wagonjwa au mmo safarini, au mmoja wenu ametoka chooni au mmewagusa wanawake, na hamkupata maji, basi tayamamuni vumbi lilio safi, na mpake nyuso zenu na mikono yenu. Hapendi Mwenyezi Mungu kukutieni katika taabu; bali anataka kukutakaseni na kutimiza neema yake juu yenu ili mpate kushukuru.
Na mwizi mwanamume na mwizi mwanamke, ikateni mikono yao, hayo ni malipo ya waliyo yachuma, ndiyo adhabu ya mfano itokayo kwa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu na Mwenye hikima.
Lakini mwenye kutubia baada ya dhulma yake, na akatengenea, basi Mwenyezi Mungu atapokea toba yake. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye maghfira na Mwenye kurehemu.
Ewe Mtume! Wasikuhuzunishe wa fanyao haraka kukufuru, miongoni mwa wanao sema kwa vinywa vyao: Tumeamini, na hali nyoyo zao hazikuamini, na miongoni mwa Mayahudi, wanao sikiliza kwa ajili ya uwongo, wanao sikiliza kwa ajili ya watu wengine wasio kufikia. Wao huyabadilisha maneno kutoka pahala pake. Wanasema: Mkipewa haya basi yashikeni, na msipo pewa haya tahadharini. Na mtu ambaye Mwenyezi Mungu anataka kumfitini huwezi kuwa na madaraka naye mbele ya Mwenyezi Mungu. Hao ndio ambao Mwenyezi Mungu hataki kuzitakasa nyoyo zao. Watakuwa na hizaya duniani, na Akhera watakuwa na adhabu kubwa.
Enyi mlio amini! Msiue wanyama wa kuwinda nanyi mmeharimia katika Hija. Na miongoni mwenu atakaye muuwa makusudi, basi malipo yake yatakuwa kwa kuchinja kilicho sawa na alicho kiuwa, katika mifugo, kama wanavyo hukumu waadilifu wawili miongoni mwenu. Mnyama huyo apelekwe kwenye Al Kaaba, au kutoa kafara kwa kuwalisha masikini; au badala ya hayo ni kufunga, ili aonje ubaya wa jambo lake hili. Mwenyezi Mungu amekwisha yafuta yaliyo pita; lakini atakaye fanya tena Mwenyezi Mungu atampa adhabu. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye nguvu na Mwenye kuadhibu.
Jueni kwamba Mwenyezi Mungu ni Mkali wa kuadhibu, na ya kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwenye maghfira, na Mwenye kurehemu.
Na pale Mwenyezi Mungu atapo sema: Ewe Isa bin Maryamu! Kumbuka neema yangu juu yako, na juu ya mama yako, nilipo kutia nguvu kwa Roho Takatifu, ukazungumza na watu katika utoto na utuuzimani. Na nilivyo kufunza kuandika na hikima na Taurati na Injili. Na ulipo tengeneza udongo sura ya ndege, kwa idhini yangu, kisha ukapuliza ikawa ndege kwa idhini yangu; na ulipo waponesha vipofu na wakoma kwa idhini yangu; na ulipo wafufua wafu kwa idhini yangu; na nilipo kukinga na Wana wa Israili ulipo wajia na hoja zilizo wazi, na wakasema walio kufuru miongoni mwao: Haya si lolote ila ni uchawi mtupu!
Na pale Mwenyezi Mungu atakapo sema: Ewe Isa bin Maryamu! Ati wewe uliwaambia watu: Nifanyeni mimi na mama yangu kuwa ni miungu badala ya Mwenyezi Mungu? (Na Isa) atasema: Subhanaka, Wewe umetakasika! Hainifalii mimi kusema ambayo si haki yangu. Ikiwa nilisema basi bila ya shaka umekwisha yajua. Wewe unayajua yaliyo ndani ya nafsi yangu, lakini mimi siyajui yaliyo katika nafsi yako. Hakika Wewe ndiye Mjuzi mkubwa wa yaliyo fichikana.