Swahili
Surah Al-Ahqaf ( The Curved Sand-hills ) - Aya count 35
Uteremsho wa Kitabu umetoka kwa Mwenyezi Mungu, Mwenye nguvu, Mwenye hikima.
Hatukuziumba mbingu na ardhi wala yaliyomo baina yake ila kwa haki na kwa muda maalumu. Na walio kufuru wanayapuuza yale wanayo onywa.
Je! Mwawaona wale mnao waomba badala ya Mwenyezi Mungu? Nionyesheni wameumba nini katika ardhi; au hao wanayo shirika katika mbingu? Nileteeni Kitabu kilicho kuwa kabla ya hiki, au alama yoyote ya ilimu, ikiwa mnasema kweli.
Na nani mpotofu mkubwa kuliko hao wanao waomba, badala ya Mwenyezi Mungu, ambao hawatawaitikia mpaka Siku ya Kiyama, na wala hawatambui maombi yao.
Na ambao watu watakapo kusanywa watakuwa maadui zao, na wataikataa ibada yao.
Na wanapo somewa Aya zetu zilizo wazi, walio kufuru husema juu ya haki inapo wajia: Huu ni uchawi dhaahiri.
Au wanasema: Ameizua mwenyewe! Sema: Ikiwa nimeizua mimi, basi nyinyi hamwezi kunifaa chochote mbele ya Mwenyezi Mungu. Yeye anajua zaidi hayo mnayo ropokwa; anatosha kuwa shahidi baina yangu na nyinyi. Na Yeye ndiye Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.
Sema: Mimi si kiroja miongoni mwa Mitume. Wala sijui nitakavyo fanywa wala nyinyi. Mimi nafuata niliyo funuliwa tu kwa Wahyi, wala mimi si chochote ila ni mwonyaji mwenye kudhihirisha wazi.
Sema: Mwaonaje yakiwa haya ni kweli yametoka kwa Mwenyezi Mungu, nanyi mmeyakataa, na akashuhudia shahidi miongoni mwa Wana wa Israili juu ya mfano wa haya, na akaamini, na nyinyi mnafanya kiburi? Hakika Mwenyezi Mungu hawaongoi watu wenye kudhulumu.
Na walio kufuru waliwaambia walio amini: Lau kuwa hii ni kheri, wasingeli tutangulia. Na walipo kosa kuongoka wakasema: Huu ni uzushi wa zamani.
Na kabla yake kilikuwapo Kitabu cha Musa, kuwa chenye uwongozi na rehema. Na hichi ni Kitabu cha kusadikisha na kilicho kuja kwa lugha ya Kiarabu, ili kiwaonye walio dhulumu, na kiwe ni bishara kwa watendao mema.
Hakika walio sema: Mola wetu Mlezi ni Mwenyezi Mungu; kisha wakatengenea, hawatakuwa na khofu, wala hawatahuzunika.
Hao ndio watu wa Peponi, watadumu humo, kuwa ni malipo kwa waliyo kuwa wakiyatenda.
Na tumemuusia mwanaadamu awatendee wema wazazi wake wawili. Mama yake amechukua mimba yake kwa taabu, na akamzaa kwa taabu. Na kuchukua mimba kwake hata kumwachisha ziwa ni miezi thalathini. Hata anapo fika utu uzima wake, na akafikilia miaka arubaini, husema: Mola wangu Mlezi! Niwezeshe nishukuru neema zako ulizo nineemesha mimi na wazazi wangu, na nitende mema unayo yapenda. Na unitengenezee dhuriya zangu. Hakika mimi nimetubu kwako, na mimi ni miongoni mwa Waislamu.
Hao ndio tunao wapokelea bora ya vitendo vyao walivyo vitenda, na tunayasamehe makosa yao. Watakuwa miongoni mwa watu wa Peponi. Miadi ya kweli hiyo walio ahidiwa.
Na ambaye amewafyonya wazazi wake na akawaambia: Ati ndio mnanitisha kuwa nitafufuliwa, na hali vizazi vingi vimekwisha pita kabla yangu! Na hao wazazi humwomba msaada Mwenyezi Mungu (na humwambia mtoto wao): Ole wako! Amini! Hakika ahadi ya Mwenyezi Mungu ni kweli. Na yeye husema: Hayakuwa haya ila ni visa vya watu wa kale.
Hao ndio ambao imehakikikishwa hukumu juu yao kama mataifa yaliyo kwisha pita kabla yao miongoni mwa majini na watu. Hakika hao wamekuwa wenye kukhasiri.
Na wote watakuwa na daraja zao mbali mbali kwa waliyo yatenda, na ili awalipe kwa vitendo vyao, na wala hawatadhulumiwa.
Na siku watakapo letwa walio kufuru kwenye Moto wataambiwa: Nyinyi mlitwaa vitu vyenu vizuri katika uhai wa duniani, na mkastareheshwa navyo. Basi leo ndio mnalipwa adhabu ya fedheha kwa mlivyo kuwa mkitakabari katika ardhi bila ya haki, na kwa sababu mlikuwa mkifanya upotovu.
Na mtaje ndugu wa kina A'di, alipo waonya watu wake kwenye vilima vya mchanga. Na kwa yakini waonyaji wengi walitokea kabla yake na baada yake kuwaambia: Msimuabudu isipo kuwa Mwenyezi Mungu. Hakika mimi nakukhofieni isikupateni adhabu ya siku iliyo kuu.
Wakasema: Je! Umetujia ili ututenge mbali na miungu yetu? Basi tuletee hayo unayo tuahidi ikiwa wewe ni miongoni mwa wasemao kweli.
Akasema: Hakika ujuzi uko kwa Mwenyezi Mungu. Mimi nakufikishieni niliyo tumwa. Lakini nakuoneni kuwa nyinyi mnafanya ujinga.
Basi walipo liona wingu likielekea kwenye mabonde yao, walisema: Wingu hili la kutunyeshea mvua! Kumbe sivyo, haya ni hayo mliyo yahimiza, upepo ambao ndani yake imo adhabu chungu!
Unaangamiza kila kitu kwa amri ya Mola wake Mlezi. Wakawa hawaonekani ila nyumba zao tu. Hivyo ndivyo tuwalipavyo wakosefu!
Na bila ya shaka tuliwaweka vizuri sio kama tulivyo kuwekeni nyinyi; na tuliwapa masikio, na macho, na nyoyo. Na hayakuwafaa kitu masikio yao, wala macho yao, wala nyoyo zao kwa lolote. Kwani hao walikuwa wakizikataa Ishara za Mwenyezi Mungu, na yale waliyo kuwa wakiyafanyia maskhara ndiyo yakawazunguka.
Na hakika tuliiangamiza miji ilio jirani zenu, na tulizitumia Ishara ili wapate kurejea.
Basi mbona wale walio washika badala ya Mwenyezi Mungu, kuwa ati hao ndio wawakurubishe, hawakuwanusuru? Bali waliwapotea! Na huo ndio uwongo walio kuwa wakiuzua.
Na wakati tulipo waleta kundi la majini kuja kwako kusikiliza Qur'ani. Basi walipo ihudhuria walisema: Sikilizeni! Na ilipo kwisha somwa, walirudi kwa kaumu yao kwenda kuwaonya.
Wakasema: Enyi kaumu yetu! Sisi tumesikia Kitabu kilicho teremshwa baada ya Musa, kinacho sadikisha yaliyo kuwa kabla yake, na kinacho ongoza kwenye Haki na kwenye Njia Iliyo Nyooka.
Enyi kaumu yetu! Muitikieni Mwenye kuitia kwa Mwenyezi Mungu, na muaminini, Mwenyezi Mungu atakusameheni, na atakukingeni na adhabu chungu.
Na wasio mwitikia Mwitaji wa Mwenyezi Mungu basi hao hawatashinda katika ardhi, wala hawatakuwa na walinzi mbele yake. Hao wamo katika upotovu ulio dhaahiri.
Je! Hawaoni ya kwamba Mwenyezi Mungu, aliye ziumba mbingu na ardhi, na hakuchoka kwa kuziumba, kuwa ni Muweza wa kuwafufua wafu? Kwani? Hakika Yeye ni Muweza wa kila kitu.
Na siku watakapo letwa makafiri Motoni wakaambiwa: Je! Haya si kweli? Watasema: Kwani? Tunaapa kwa Mola wetu Mlezi, ni kweli! Atasema: Basi onjeni adhabu kwa sababu ya kule kukataa kwenu.
Basi subiri, kama walivyo subiri Mitume wenye stahmala kubwa, wala usiwafanyie haraka. Siku watakayo yaona waliyo ahidiwa itakuwa kama kwamba hawakukaa ulimwenguni ila saa moja ya mchana. Huu ndio ufikisho! Kwani huangamizwa wengine isipo kuwa walio waovu tu?